Safari kwenye nyika za Kenya
Kaskazini mwa Mlima Kenya kwenye kingo za Mto Ewaso Nyiro, kuna Mbuga ya Wanyama ya Samburu. Tembo wa eneo hili wamefanyiwa utafiti na shirika la Save the Elephants kwa zaidi ya miaka 20. Jifahamishe kuhusu mandhari, watu na wanyamapori wa Samburu.
Kuelewa na kuwalinda tembo
Tembo Waliotambulika Kibinafsi
1,450
Ukaguzi wa Nyanjani Uliorekodiwa
20,655
Saa za Ufuatiliaji wa GPS
845,000
Hapa unaweza kumwona Pilipili kutoka Familia ya Viungo. Jamii za tembo hupewa majina yanayodhihirisha sifa moja (k.m., Ufalme) na kisha kila mwanajamii hutajwa jina kulingana na sifa hiyo (k.m., Elizabeth, Henry, Noor). Tembo wachanga hutambuliwa kwa misimbo ya nambari kulingana na mama ao na tarehe ya kuzaliwa. Nyuma ya Pilipili unaweza kumwona ndama wake mwenye umri wa miaka 5 ambaye msimbo wake ni M63.9410. Gundua eneo hili.
Ndume huyu mwenye umri wa miaka 16 ni mwanawe Ebony (mti wa Mpingo kwa Kiingereza), wa jamii ya Mitimigumu ambaye alishikwa mwaka wa 2011. Unaweza kuwatambua tembo wa kiume kutokana na vichwa vyao vya mviringo na miili mikubwa. Tembo wa kiume wanapokua, huingia katika jamii ya tembo dume. Tembo wa kiume hujiitenga na familia zao na kutumia muda mwingi wakiwa na ndume wengine au wakitafuta wenza wa kike. Akiwa na umri wa takribani miaka 30, ndume ataanza kuingia katika kipindi cha ujasiri mara kwa mara, ambapo huonyesha uwezo wake wa uzazi. Gundua sehemu mbalimbali za eneo hili
Tembo hupenda kuishi pamoja na hutumia muda mwingi wakiwa katika familia zao wenyewe na tembo wengine. Wanaweza kuwatambua mamia ya tembo wengine. Upande wa kushoto ni Alto wa familia ya Mawingu akiwa na ndama wake, naupande wa kulia ni Habiba kutoka Swahili Ladies (angalia ukanda wake wa shingoni wa GPS Baada ya mamake kuuawa, Habiba alibaki yatima na kujiunga na familia ya Viungo hadi alipozaa ndama wake. Unaweza kuona ndama wake wa kike katika mandharinyuma, akiwa pamoja na Layla na ndama wake kutoka jamii ya Wanawake Waswahili. Gundua eneo hili.
Jifahamishe kuhusu jamii ya tembo kutoka Samburu
Muundo wa familia ni muhimu zaidi kwa tembo, na kuhifadhi familia ni muhimu katika kuongeza idadi ya tembo. Shirika la Save the Elephants limetambua na kufuatilia zaidi ya jamii 70 za tembo eneo la Samburu. Wafahamu vizuri.
Kulinda tembo wa Kenya
Tatizo la ujangili limekumba Afrika katika miaka ya hivi karibuni. Hii imesababisha vifo vya zaidi ya tembo 100,000 kati ya mwaka wa 2010 na 2012. Makundi ya watu na mashirika yamejitolea kuungana ili kuwalinda. Pata maelezo kuhusu juhudi za kudumisha mustakabali wa tembo wa Afrika.
Kuwekwa mikanda shingoni
Kuwekwa mikanda shingoni
Shirika la Save the Elephants hutumia mikanda GPS ili kufuatilia tembo nyikani. Kufuatilia tembo husaidia shirika kubaini jinsi tembo wanavyotembea, kukagua mabadiliko katika tabia zao na kudumisha usalama wa kila tembo. Shirika la Save the Elephants (STE) limewawekea jumla ya tembo 266 mikanda kote barani Afrika.
Ufuatiliaji.
Ufuatiliaji.
Ufuatiliaji wa tembo hufanyika ardhini, angani na kupitia GPS. Watafiti hutumia muda mwingi kuandika maelezo ya kina kuhusu tabia na mwendo wa tembo, na wakiwa katika sehemu kama vile Hifadhi ya Wanyamapori ya Lewa data kutoka tembo walio na mikanda huwekwa kwenye Google Earth ili kufuatilia tembo katika wakati halisi.
Kushika oria
Kushika oria
Kuna juhudi zinazofanywa ili kudumisha mustakabali wa tembo katika Afrika. Katika eneo la Samburu, mbwa waliofunzwa hutumika kufuatilia majangili mwituni. Shirika la Huduma kwa Wanyamapori la Kenya (KWS) askari wa Hifadhi ya Kitaifa ya Samburu na jumuiya ya hifadhi ya Nothern Rangelands Trust zimekuwa zikishirikiana ili kukabili majangili. Mashirika hayo yamefaulu, na katika mwaka wa 2014, kwa mara ya kwanza tangu tatizo la ujangili lianze miaka sita iliyotangulia, idadi ya tembo waliozaliwa ilizidi idadi ya tembo waliouawa. Mapambano yanaendelea kila mahali katika Afrika.
Utunzaji
Utunzaji
Shirika la David Sheldrick Wildlife Trust lina jukumu la kulinda wanyamapori wa Afrika waliohatarishwa, wakiwemo tembo. Kupitia Mradi wa Wanyama Mayatima mjini Nairobi, shirika hili lina jukuma la kuwatunza tembo waliojeruhiwa au mayatima kabla ya kuwarejesha porini. Tembo wachanga hutunzwa na mlinzi kwa saa 24 kwa siku, jambo ambalo huwasaidia kuingiliana vizuri na kuongezeka uwezekano wa kuishi peke yao wanapoachiliwa kurejea porini.
Kupanga
Kupanga
Tembo wa Samburu husafiri kwenye mandhari, wakitoka mahali pamoja hadi pengine kupitia njia nyembamba ardhini zinazoitwa 'mapito.' Mara nyingi, safari zao kupitia mapito haya zinahatarishwa na binadamu na magari. Kutokana na data ya GPS iliyotolewa na Save the Elephants, shirika la Mount Kenya Trust lilitenga ardhi na kufadhili ujenzi wa njia za chini ya barabara kuu ili tembo waweze kuzipitia.
Hifadhi ya Kitaifa ya Samburu ni eneo linalolindwa katika sehemu ya kaskazini mwa Kenya. Inachukua muda wa takribani saa 6 kusafiri kwa gari kutoka Nairobi. Mandhari katika hifadhi yanaweza kuwa na misitu, nyika na milima. Mto wEwaso Nyiro hupitia mpaka wa Kusini wa hifadhi na ndio chanzo cha uhai katika eneo hili. Maji yake hutumiwa na watu, mimea na wanyama.
Samburu ni eneo lenye wanyamapori wengi. Lina mandhari ya joto, nyika, ardhi tambarare na mto. Miezi ya Februari na Machi ndiyo huwa na joto jingi zaidi, ikifuatwa na misimu miwili ya mvua katika mwaka. Mandhari kame huwa na mimea ya mitende kwenye changarawe, na kwa umbali, unaweza kuona milima ya Koitogor na Olelokwe.
Wageni huzuru eneo la Samburu ili kuangalia tembo, chui, simba, twiga na zaidi ya aina 450 za ndege. Jambo la kipekee katika eneo hili ni pundamilia wa Grevy wanaotambulika kwa milia yao miembamba, masikio makubwa yaliyoviringa na miili mikubwa. Wakati wa ziara ya kutazama wanyama, unaweza kuona mbuni wa Kisomali, mamba wa Nile na kundi kubwa la paa aina ya choroa, wote wanaweza kuishi jangwani na hupenda mazingira yenye joto kama haya. Gundua sehemu mbalimbali za eneo hili.
Samburu inajulikana kwa kuwa na idadi kubwa sana ulimwenguni ya tembo waliofanyiwa utafiti. Kutokana na miaka 20 ya utafiti, tembo wa eneo hilo wanaaminika sana na huweza kukaribia magari, haswa lori la watafiti wa Save the Elephants. Tembo wanaweza kukumbuka mambo kwa muda mrefu. Wao huelewa mipaka ya Hifadhi ya Samburu na huonyesha tabia tulivu wakiwa katika eneo lililolindwa. Gundua sehemu mbalimbali za eneo hili
Tembo hutekeleza jukumu muhimu zaidi kama wahandisi wa mandhari katika mazingira. Husaidia katika usambazaji wa mbegu kwa kula matunda kutoka miti na kisha kueneza mbegu kupitia samadi zao. Tambo hupasua magamba ya miti, hukata mimea na kusababisha mimea kukua tena na kusambaza mbegu nyingi. Wakati wa kiangazi, tembo huchimba mashimo kutafuta maji ambayo hutumiwa baadaye na wanyama wengine. Tembo wana athari kubwa sana katika mandhari.
Shirika la Save the Elephant lilianzishwa mwaka wa 1993 na limejitolea kulinda mustakabali wa tembo na kudumisha hadhi ya ekolojia katika eneo wanakoishi. Makao makuu ya shirika la STE ni Nairobi na linafanya kazi Afrika kote ili kuelewa na kulinda tembo. Kituo kikuu cha utafiti kiko Samburu, ambako tembo hufuatiliwa kupitia nchi kavu, angani na kwa kutumia mbinu ya GPS. Wao huangazia utafiti kama msingi ambapo wanaweza kufanya maamuzi ya mipango na kuunda sera na kujitahidi ili kuboresha uhusianao uliopo kati ya binadamu na tembo. Gundua eneo hili.
Katika miaka ya 1960, mwanabayolojia aliyeitwa Iain Douglas-Hamilton alianzisha utafiti wa kwanza wa kitabia wa tembo wa porini nchini Tanzania, kwa kutumia ndege ndogo ya kuwafuatilia na kuwahesabu. Mwaka wa 1993 alianzisha shirika la Save the Elephants, na kisha akachagua tembo wa kipekee walio wapole na wanaoamini wa Samburu kama somo katika utafiti mpya wa muda mrefu kuhusu tembo. Utafiti uliofanywa Samburu huleta ufahamu wa kimataifa wa vitisho kwa tembo na huleta ufumbuzi wa kuhakikisha usalama wa tembo kwa ajili ya kizazi kijacho.
Shirika la Save the Elephants linafanya uchuguzi wa angani kuhusu tembo na pia kufuatilia kila tembo kwa kutumia mikanda ya GPS. Kwa kumweka tembo katika hali ya nusu kaputi kwa haraka, daktari wa wanyama huweka mkanda kwenye shingo la tembo ili kufuatilia mahali alipo. Data hii huwasaidia watafiti kuelewa jinsi wanyama hawa hutembea mbugani, na pia kuchunguza maisha ya tembo mahususi. Kwa kuchunguza data ya GPS, shirika la Save the Elephants linaweza pia kupata kiotomatiki arifa za kuonyesha kuwa mnyama ameacha kutembea. Kufikia sasa STE imewawekea jumla ya tembo 266 mikanda kote barani Afrika.
STE ilikuwa ikikusanya data nyingi kutoka mikanda ya GPS iliyowekwa kwenye tembo, lakini ilihitaji njia ya kuichanganua. Katika mwaka wa 2006, STE ilianza kuweka data ya mikanda kwenye mandhari makubwa ya dijitali ya Google Earth, ili kuruhusu ufuatiliaji bora wa miendo ya tembo. Kwa sasa inatumia uwezo wa kitarakilishi wa Google Earth Engine, ili kuchanganua zaidi ya maeneo milioni tano yaliyorekodiwa kutoka tembo 266 kwa zaidi ya miaka 17.
Tembo hutembea popote na mara nyingi hukutana na barabara, nyumba, mashamba na watu. Mgogoro kati ya watu na tembo ni tatizo kubwa katika ulinzi wa tembo, na mbinu moja ya kuhifadhi tembo ni kuwatengenezea njia salama. Kwa kutumia data ya ufuatiliaji wa tembo, njia hizi za chini ya barabara kuu zilitengenezwa ili kuwaruhusu tembo kutembea kwa usalama chini ya barabara hii kuu. Gundua eneo hili
Ujangili ndio hatari kubwa zaidi inayokabili maisha ya tembo katika Afrika. Tembo huuawa kwa ajili pembe zake ambazo huuzwa ulimwenguni kote. Tembo waliokomaa wakiuawa huacha athari kubwa katika familia zao na husababisha ndama wengi kuwa mayatima. Vita dhidi ya ujangili vinahitaji adhabu kali kwa majangili na pia kuzuia matumizi ya bidhaa zinazotokana na pembe za tembo.
Kifo cha tembo ni hasara kubwa katika utamaduni wa Wasamburu. Ujangili husababisha ukosefu wa uthabiti katika maisha ya watu wanaoishi pamoja na tembo, wakati tembo wanapouliwa kwa ajili ya pembe. Mpango wa Northern Rangelands Trust unahusisha wenyeji katika kuhifadhi, kubadilisha ardhi kuwa mbuga za wanyama, kuunda nafasi za kiuchumi kupitia utalii, na hata kuonyesha thamani ya tembo katika eneo la Samburu.
Askari wa pori wamejitolea kupambana na majangili na huhatarisha maisha yao wakilinda tembo wa Kenya. Wao hudokezewa na wenyeji na mashirika na kisha husaka mbuga wakiwa na mbwa waliofunzwa kutafuta shughuli haramu. Kazi bora ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Lewa na Shirika la Huduma kwa Wanyamapori la Kenya imesaidia kupunguza idadi ya tembo waliouawa katika sehemu ya Kaskazini mwa Kenya kufika chini ya asilimia 1 ya idadi ya jumla. Huu ni ushindi mkuu katika vita vya kulinda tembo.
Ndama wa tembo hufanyaje wakati tembo ameuliwa? Shirika la David Sheldrick Wildlife Trust lilianzishwa mwaka wa 1977. Jukumu lake ni kutoa usaidizi kwa wanyama wanaohitaji msaada, wakiwemo mayatima. Katika kituo chao cha kutunza wanyama yatima mjini Nairobi, walinzi huwalisha na kuwafanyiza mazoezi tembo na kuhakikisha kuwa wamejumuishwa vizuri katika kundi la mayatima. Aina hii ya utunzaji ni muhimu katika kuwalea tembo wenye afya bora wanaoweza kurejeshwa tena porini. Sheldrick Trust imelea ndama wa tembo zaidi ya 180 waliohudumiwa kwa mkono. Gundua eneo hili
Katika mwaka wa 2012, STE iliomba kwa mara ya kwanza Trekker ya Taswira ya Mtaa iletwe eneo la Samburu ili kupiga picha za digrii 360 za tembo katika pori. Si kila mtu anaweza kutembelea Samburu, lakini kila mtu anaweza kufanya safari ya mtandaoni ili kuwaona tembo hawa. Kwa kufanya tembo waonekane kwa urahisi mtandaoni, watafiti na watetezi wanatarajia kuwa watu wataweza kuwatazama zaidi tembo na kufurahi zaidi kushiriki katika kulinda mustakabali wao.
Kuokoa tembo wa Samburu
Hadithi za Wasamburu zinasimulia asili ya pamoja kati ya watu na tembo, na kwa miaka 120 iliyopita, eneo hili limekuwa makao ya STE. Gundua jinsi utafiti unaotumia data umebadilisha uhifadhi wa tembo.
Ujumbe kutoka kwa
Iain Douglas-Hamilton
Niliingia katika ulimwengu wa ajabu miaka 50 iliyopita wakati nilianza kufanya utafiti kuhusu tembo wa Ziwa Manyara, Tanzania. Maisha yangu yalizingirwa na wanyama hawa wa kupendeza na mandhari mazuri ambako wanaishi -- misitu mikubwa, ardhi tambarare, mito, maziwa, volkano na mitiririko ya lava, kuanzia misituni hadi jangwani na hata keleleni mwa milima.
Samburu ni mojawapo ya mandhari haya, na ni muhimu sana kwangu kwa kuwa hapa ni nyumbani. Nina furaha kushiriki mahali ninapopenda kwenye Taswira ya Mtaa, na kuruhusu watu kutoka kila mahali watazame tembo katika ziara ya utambuzi mtandaoni. Tunatarajia kuwa kupatikana kwa eneo hili kwenye Ramani za Google na Google Earth kutakufanya ufahamu zaidi kuhusu tembo, jambo ambalo linaweza kukufanya uchukue hatua ya kuwalinda.
Tembo na wanyama wengine wa pori wanahitaji msaada wetu. Tunapaswa kuruhusu umaridadi wa maumbile udumu pamoja nasi. Tuliwaleta tembo wa Samburu mtandaoni ili watu waweze kuwatazama, kufurahia makao yao na kutambua kuwa kuna haja ya kuchukua hatua za dharura ili kuwalinda. Kadri tunavyowaelewa wakazi wa ulimwengu halisi, ndivyo tunavyoweza kuwasaidia waishi katika sayari hii. Ungana nasi ili tujitahidi kuwalinda tembo wa Afrika.
—Iain Douglas-Hamilton, PhD, CBE
Mwanzilishi wa, Save the
Elephants
September 15, 2015
Jifahamishe na Save the Elephants
Kwa kutumia utafiti wa angani na mikanda ya GPS, STE ndilo shirika maarufu zaidi linalohusika na utafiti wa tembo ulimwenguni. Kutana na kundi lenye bidii la wanasayansi na watetezi ambao wamejitolea kudumisha mustakabali salama wa tembo.
Pata maelezo zaidi
Shirika la STE limejitolea kulinda mustakabali wa tembo, kudumisha hadhi ya
kiokolijia ya maeneo wanakoishi, kuwafanya binadamu wafurahie akili na sifa
mbalimbali za tembo, na kuendeleza uhusiano bora kati ya binadamu na tembo.
savetheelephants.org
Shirika la David Sheldrick Wildlife Trust lilitokana na ari ya familia moja kuhusu nchi ya Kenya na wanyamapori wake. Kwa sasa, huu ndio mpango uliofaulu zaidi ulimwenguni wa kuwaokoa tembo yatima na kuwatunza. Pia, ni mojawapo wa mashirika ya kwanza ya kuhifadhi wanyamapori na makao yao katika Afrika Mashariki. sheldrickwildlifetrust.org
Hifadhi ya Wanyamapori ya Lewa ni mpango bora zaidi wa hifadhi ya jamii, Eneo la Turathi za Kimataifa la UNESCO na inapatikana katika Orodha ya Kuhifadhi Mazingira Asili ya Umoja wa Kimataifa ya maeneo yaliyolindwa vizuri. Lewa ni nguzo muhimu katika kuhifadhi wanyamapori, kudumisha maendeleo na kukuza utalii unaofaa katika sehemu ya kaskazini mwa Kenya. lewa.org
Eneo la Samburu limekuwa na watu tangu asili ya binadamu na serikali ya eneo hiyo imejitolea kuboresha masilahi ya watu, wanyama na mandhari ya kijiografia katika eneo hili. Kwa kufanya miradi inayoangazia uchumi, miundomsingi, elimu na ulinzi wa wanyamapori, serikali ya Samburu imejitolea kuongeza ufikiaji katika eneo na usalama. samburu.go.ke
KWS imejitolea kuhifadhi aina za wanyama wakuu wanaosalia na maeneo kwa ajili ya
vizazi vijavyo. Shirika hufanya kazi kwa bidii ili kuhifadhi, kudhibiti na
kuwalinda, na kuongeza wanyamapori wa Kenya, makao yao na kutoa huduma mbalimbali
kwa ushirikiano na washikadau ili kudumisha maisha.
kws.go.ke
Google Earth Outreach ni mradi ulioanzishwa kusaidia haswa mashirika yasiyo ya faida na yale yanayofaidi umma kote duniani kutumia uwezo wa Google Earth na Ramani za Google kuonyesha na kutetea kazi muhimu inayofanywa na mashirika hayo. Miradi ya Uhisani wa Google Earth huangazia mazingira, kuhifadhi tamaduni, kazi za uhisani na mengine. google.com/earth/outreach